Kampeni ya usafi kwa Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi inayojulikana kama "Safisha, Pendezesha Dar es Salaam" imefanyika kwa kishindo ambapo imeongozwa na mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe. Hashim Komba.
Zoezi hilo limefanyika mapema leo jumamosi ya Machi 25, 2023 katika eneo la kituo cha Daladala cha Malamba Mawili kata ya Msigani ambapo taasisi mbambali ikiwemo Chama Cha Mapinduzi CCM, benki ya NMB na CRDB pamoja wananchi wa maeneo hayo wamejitokeza kwa wingi.
Wakati akiongea na wananchi hao Mh. Komba kwanza amewapongeza kwa kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni hiyo ya usafi na pia ametoa maagizo kwa wale wote ambao wanakusanya michango kwa wafanyabiashara ambao wanafanya shughuli zao kwenye maeneo ambayo sio rasmi
"Nafahamu kuna wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanafanya shughuli zao kwenye maeneo ambayo sio rasmi. Sasa wakati taratibu za kuwahamisha kwenda kwenye maeneo rasmi zinaendelea kati ya Manispaa, TANROAD na Wafanyabiashara, kuna watu wachache wanachangisha michango mbalimbali kwa wafanyabiashara hao kinyume na sheria. Nitamke hapa napiga marufuku michango yote isipokuwa mchango wa usafi tu" Amesisitiza mhe. Komba
Aidha Mhe. Komba amesikitishwa na kitendo cha madereva bajaji wa eneo hilo kutoshiriki zoezi hilo la usafi, hivyo ametoa maelekezo kuwa viongozi wa madereva bajaji, OCD, LATRA na Afisa biashara wafike ofisini kwake jumatatu asubuhi.
Pia ameagiza jumamosi ijayo ya Aprili 01, 2023 zoezi la usafi wa eneo hilo utaongozwa na madereva bajaji.
Awali akitoa salamu za Manispaa na baraza la Madiwani, mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe. Jaffary Nyaigesha amewapongeza wananchi wote waliojitokeza kwenye usafi na amewataka kuhakikisha zoezi la usafi inakuwa ni utamaduni wao wa kila siku kwenye maeneo yao ya biashara na makazi pia.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa