Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) azitaka Wizara ya TAMISEMI na wizara ya Ardhi kutenga maeneo ya Uwekezaji kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji Nchini.
Sambamba na hilo amewataka Watanzania kuthamini uwekezaji mkubwa unaofanyika Ubungo na maeneo mengine na kuwaasa vijana wanaopata ajira kwenye miradi mbalimbali ya uwekezaji na amewataka wawekezaji kuzingatia Watanzania wote waliawajiri wanapata stahiki zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Nchi yetu.
Maelekezo hayo ameyatoa leo tarehe 20/04/2023 wakati anakagua mradi wa ujenzi wa kituo cha biashara cha kimataifa kinachojengwa katika manispaa ya ubungo eneo la stendi kuu ya zamani ya mabasi yaendayo mikoani.
Mhe. Majaliwa ameendelea kueleza kuwa kituo hicho kina maslahi makubwa kwa wananchi wa Ubungo na Taifa kwa ujumla kwani kitaenda kuchochea ongezeko la ajira, ukuaji wa uchumi kwani mapato ya Manispaa ya Ubungo yataongezeka na ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kuchangamkia fursa ya uwepo wa kituo hicho cha kimataifa cha kibiashara.
“Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji hapa nchini kutoka ndani na nje ya nchi na itaendelea kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyopo hapa nchini kwa maslahi mapana ya watanzania” alisema Mhe. Majaliwa
Akiongea Mhe. Anjella Kairuki Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI amesema mnamo tarehe 16/12/2023 Manispaa ya Ubungo iliingia mkataba na kampuni ya Shanghai Linghang group limited ambae ni mwekezaji aliyewekeza kwenye eneo la Ubungo ilipokuwa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani kwa ajili ya kujenga kituo cha kimataifa cha kibiashara na mkataba huo kila baada ya miaka mitatu utafanyiwa marejeo na mapitio na kuboreshwa kwa mujibu wa bei za soko.
Mhe. Kairuki ameendelea kueleza kuwa uwekezaji huo unathamani ya dola 81,827,655.01 sawa na fedha za kitanzania shilingi bilioni 195 na mwekezaji atakuwa amerejesha fedha za uwekezaji baada ya muda wa uwekezaji kuisha na atatakiwa kukabidhi umiliki wa asilimia 100 kwa Manispaa ya Ubungo.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema kituo hicho kitazalisha ajira rasmi za moja kwa moja zaidi ya 15,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 50,000 na kitakuwa na maduka ya ukubwa tofauti tofauti zaidi ya 2,000 na pia wafanyabiashara watapata fursa ya umiriki wa moja kwa moja wa maduka yao.
Kampuni ya Shanghai Linghang group limited imeiteua kampuni ya EAST AFRICA COMMERCIAL & LOGISTICS CENTER (EACLC) kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, alieleza Mhe. Kairuki
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya EACLC Ndg. Catty Wang ameishikuru Serikali ya Tanzania kwa kuipa kibali cha ujenzi wa mradi huo na kusema mradi huo utakamilika mnamo mwezi Juni 2024 na mara moja biashara ziataanza kufanyika.
Catty amesema mradi huo utakuza biashara ndogo ndogo na kupanua biashara hizo ndani ya soko kubwa la Afrika kwani watanzania watapata fursa ya kuagiza na kuuza bidhaa nje ya Tanzania.
“Katika kuendesha uwekezaji wetu Nchini Tanzania kampuni ya EACLC limited itaendelea kutekeleza misingi ya ukweli, matokeo ya uhakika na imani njema kuhusu ushirikiano na Afrika ambao ni msingi uliowekwa na Mhe. Rais wa China Xi Jinping alipokuwa Dar es salaam miaka 10 iliyopita na pia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa Nchini China hivi karibuni” aliahidi Wang.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa