Mashindano ya UMISETA wilaya ya Ubungo yaliyokua yakifanya katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola iliyopo Mabibo, yamefungwa rasmi leo kwa timu ya kanda ya Ubungo kuibuka mabingwa.
Mashindano hayo yalikua yakishirikisha timu za shule mbalimbali za Wilaya ya Ubungo ambapo zilichujwa na kupatikana timu tatu za kanda tatu ambazo ni kanda ya Kibamba, Kanda ya Goba na kanda ya Ubungo ambapo baada ya hatua mbalimbali za mashindano hayo leo Juni 17 ilikua ni fainali kati ya kanda ya Kibamba dhidi ya kanda ya Ubungo.
Mashindano hayo yalikua ni maalumu ili kuchagua wanafunzi watakaounda timu ya Manispaa ya Ubungo ambayo itaenda kushiriki mashindano ya mkoa yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 26 mpaka Julai 30, 2022.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Afisa elimu sekondari Manispaa ya Ubungo ndugu Voster Mgina amesema kuwa mashindano hayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa kwa sababu wilaya ya Ubungo ina vijana wenye vipaji vikubwa katika michezo mbalimbali na kuwa timu ya Wilaya iliyopatikana ni nzuri na matumaini ni kuwa itaenda kufanya vizuri kwenye mashindano ya mkoa
Naye mgeni rasmi wa mashindano hayo meneja wa benki ya NMB tawi la chuo kikuu cha Dar es salaam, ndugu Msafiri Hamza Mfinanga amesema kuwa mashindano ya michezo kwa wanafunzi mashuleni ni jambo muhimu sana kwa afya ya mwili na akili kwa wanafunzi hao na wao kama benki wataendelea kushirikiana na serikali kwenye programu mbalimbali za michezo kwa wilaya ya Ubungo.
"Benki ya NMB ipo karibu na watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi hivo basi wataendelea kuwa karibu na jamii kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo misaada ya vifaa vya michezo kwa wanafunzi" alisema.
Aidha, Afisa utamaduni Manispaa ya Ubungo ndugu Kassim Semfuko amewapongeza wakuu wa shule mbalimbali za Manispaa ya Ubungo kwa usimamizi mzuri wa mashindano hayo kuanzia mwanzo mpaka mwisho na pia amewapongeza wanamichezo wanafunzi walioshiriki kwenye mashindano hayo na pia amewasihi kuendelea kulinda vipaji vyao ili siku moja vije kuwa ajira kwao na pia kuleta mchango mkubwa kwa taifa letu.
#UbungoYetuFahariYetu
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa